Πέμπτη 29 Οκτωβρίου 2015

Uharamia Afrika Magharibi

dw.com

Tunapozungumza kuhusu uharamia barani Afrika hii leo, fikra ya kila mmoja huelekea Somalia. 

Cotonou, mji mkuu wa Benin

Lakini pwani ya Afrika magharibi imegeuka kuwa eneo la pili hatari kwa maharamia wanaolenga hususan mafuta na meli za kemikali wakitumia silaha za kutegeshwa na miripuko ya roketi.´
Uharamia katika pwani ya Afrika magharibi unaongezeka katika kiwango cha kushtusha na unatatiza vibaya mpangilio wa biashara ya kimataifa. Pwani ya Afrika magharibi imeshuhudia zaidi ya mashambulio 20 dhidi ya meli za kemikali na za mafuta katika nusu ya kwanza ya mwaka huu [2011].
Nchi ya Benin peke yake imeripoti visa 15. Vyombo sita vya baharini vimetekwa nyara. Maharamia waliwalazimisha manahodha wa meli kuzielekeza meli zao katika maeneo yasiyojulikana, ambapo mizigo kwenye meli hizo yaliibiwa, huku mabaharia kadhaa wakijeruhiwa.

Bandari ya Cotonou, Benin

Maxime Ahoyo ni kamanda wa jeshi la majini la Benin. Anasema serikali nyingi katika eneo hilo zina wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulio hayo. Na ndiyo sababu serikali ya Benin imeamua kuliongeza nguvu jeshi lake la majini.
' Tunatarajia ndege mbili za kijeshi zilizo na kamera za kuweza kuona usiku. Ndege hizo ndogo zinapangwa kuwasilishwa mwezi Septemba kutoka Ufaransa. Na Boti tatu za kupiga doria zinatengenezwa Ufaransa. Zitawasili mwezi Februari mwaka 2012'.
Ahoyo anaeleza kuwa punde tu boti hizo zitakapowasili mwezi huu, Benin itaimarisha usalama katika bahari yake. Boti hizo zitaweza kusafiri kwa umbali mkubwa na zitaweza kusafiri haraka katika bahari kubwa ambapo maharamia huzitegesha meli zao ili kuweza kuiba mizigo.
Pottengal Mukundan ni mkurugenzi wa ofisi ya kimataifa ya ubaharia nchini Uingereza na anaeleza kuwa njia ambazo meli zinatekwa nyara Afrika magharibi ni sawa na kama ilivyo Afrika mashariki.
'Wanatumia mbinu sawa za mashambulio, wanajitokeza kwenye viboti vidogo, na silaha za kutegeshwa na miripuko ya roketi na huzilazimisha meli kupunguza kasi au kusimama, na baada ya hapo wanapanda kwenye meli hizo'.
Hata hivyo maharamia katika Afrika ya magharibi, wana malengo tofauti na wenzao wa Somalia. Maharamia wa Somalia huziteka meli na mabaharia waliomo kwenye meli hizo, na baadaye wakadai malipo ya fedha ili wawaachilie. Kwa upande wa maharamia wa Afrika magharibi, maharamia hao huiba mizigo iliyomo kwenye meli hizo, nayo huwa ni mafuta na mitungi ya gesi ambayo huyauza katika soko haramu. Bamidele. A. Ojo, ni mtaalamu wa masuala ya kigaidi katika chuo kikuu cha Dickinson nchini Marekani.
'Unapokuwa na shughuli za kihalifu ambazo zinaathiri usafirishaji mafuta, ina maana kuwa ni lazima uzidishe usalama katika meli, ni lazima uongeze hatua za kiusalama kuziongoza meli hizo wakati zinaposafirisha mafuta ghafi kutoka Afrika magharibi hadi Ulaya, na hilo bila shaka litaongeza thamani ya mafuta na bei itaweza kuwasilishwa kwa watu binafsi katika eneo la Ulaya ya magharibi na Marekani'.
Hata hivyo vyombo vya habari vya kimataifa havijaangazia ongezeko la visa vya uharamia katika pwani hiyo ya Afrika magharibi. Serikali za Afrika magharibi zinafikiria kuwa mpango wa pamoja ni suluhu iliyo bora kukabiliana na mashambulio ya maharamia.
Hata hivyo wataalamu wanasema inahitaji jitihada zaidi, kuliko ununuzi wa boti mpya za kupiga doria kwa jeshi la majini katika eneo hilo. Na wanasema huenda mfumo huo wa pamoja wa ulinzi usiwepo hivi karibuni kwa kuwa nchi katika eneo hilo ni maskini mno kuweza kuugharamia.

Mwandishi: Alice Kiingi/ Maryam Abdalla
Mhariri:Josephat Charo

Ona pia

Δεν υπάρχουν σχόλια:

Δημοσίευση σχολίου